Thursday, March 24, 2016

USTAWISHAJI WA ZAO LA KABICHI




 Zao la kabichi hulimwa katika mikoa ya Morogoro, Arusha,Tanga, Iringa, Kilimanjaro na Mbeya. Kama mboga zao la kabichi lina viini lishe kama chokaa, protini, kambakamba na maji kwa wingi. Hutumika kutengeneza kachumbari, pia kuchanganywa na nyama au maharage.

HALI YA HEWA
Zao la kabichi hupendelea: hali ya ubaridi Mwinuko: Kuanzia mita 1200 hadi 1900 kutoka usawa wa bahari. Udongo uwe; Tifutifu,  Rutuba nyingi na Unaohifadhi unyevu kwa muda mrefu, Usiotuamisha maji , Usio na chumvichumvi nyingi. Kama hauna rutuba ya kutosha ongeza mbolea ya samadi au mbolea vunde. 

 AINA ZA KABICHI
 Early Jersey Wakefield:  Umbo lilochongoka kidogo, Hufunga vizuri,  Uzito ni kati ya kilo 1.5 hadi 2.0,  Hukomaa mapema siku 90 – 100 tangu kupandikiza. · Copenhagen Market: Vichwa vya mviringo na hupasuka kirahisi . Hukomaa mapema, siku 90 – 100 tangu kupandikiza ·
 Prize Drumhead: Vichwa vikubwa (kilo 2- 2.5), Vichwa ni bapa, huchelewa kukomaa (siku 110 – 120) - Huvumulia hali ya jua kali, Pia vichwa hupasuka. · Oxheart: - Vichwa vidogo huchongoka kama moyo,  Hupendwa sana na walaji,  Ladha yake ni tamu, hukomaa mapema, Hazina tabia ya kupasuka.  Glory of Enkhuizen: - Vichwa vya mviringo, Huvumilia hali ya jua kali,  Huchelewa kukomaa (siku 110 – 120)  na  Ina tabia ya kupasuka.

KUOTESHA MBEGU
Mbegu za kabichi huoteshwa kitaluni na baadaye huhamishiwa shambani. Andaa kitalu vizuri na weka mbolea za asili zilizooza vizuri kwa kiasi cha ndoo 5 – 10 za ujazo wa kilo 20 kwenye eneo la mita za mraba 10. Changanya na udongo kisha lainisha udongo kwa kuvunja mabonge makubwa kwa kutumia reki. Tengeneza tuta lililoinuka kwa sentimita 25 na lenye upana wa mita 1.
Mwagilia maji kwenye tuta siku moja kabla ya kusia mbegu. Kiasi cha mbegu zinazohitajika ni gramu 1 kwenye eneo la mita 1 ya mraba hivyo hekta 1 huhitaji gramu 200 – 300. Sia katika umbali wa sentimita 15 toka mstari hadi mstari na kina cha nusu sentimita.Funika mbegu na udongo laini kasha tandaza nyasi kazu ili kuhifadhi unyevu.Mwagilia maji kila siku asubuhi na jioni mpaka mbegu ziote, huota kwa muda wa siku 5 – 10.

KUTAYARISHA SHAMBA
Shamba litayarishwe mwezi mmoja kabla ya kupandikiza.
·        Katua ardhi kwa kina cha sentimita 30
·        Lainisha udongo na tengeneza matuta  kisha weka mbolea za asili kwa kiasi cha ndoo 2 kwa kila hatua moja au Mbolea iwekwe kwa kila shimo kwa kiasi cha kilo kwa shimo.
·         Mbolea ya N.P.K. 5:15:5 yaweza kuwekwa kwa kiasi cha kijiko 1 cha chai chenye gramu 5 kwa kila shimo.


KUPANDIKIZA MICHE

 
 
 Miche huwa tayari kupandikizwa shambani baada ya wiki 3 – 5 tangu kusia mbegu . Miche huwa na urefu wa sentimita 15 – 20. Ng’oa miche kwa uangalifu na pandikiza kama ilivyokuwa kitaluni na hakikisha mizizi haipindi wakati wa kupandikiza. Nafasi ya kupandikiza: Hutegemea aina ya kabichi – zenye vichwa vikubwa (Drumhead) ni sentimita 60 kutoka mche hadi mche na sentimita 75 toka mstari hadi mstari. – Zenye vichwa vidogo (Oxheart) ni sentimita 40 – 50 kutoka mche hadi mche na sentimita 60 toka mstari hadi mstari. – Umbali toka tuta moja na jingine ni sentimita 60. – Muda mzuri wa kuotesha ni asubuhi au jioni – Baada ya kupandikiza weka matandazo kama vile nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu na kuzuia magugu kuota kwa urahisi. 

 PALIZI
 Zao la kabichi halina mizizi ya kina kirefu hivyo wakati wa palizi ni muhimu kuwa mwangalifu kwa kupalilia juu juu ili kuepuka kukata mizizi. Kuongeza matandazo husaidia kupunguza palizi a mara kwa mara.

UMWAGILIAJI
 Kabichi hustawi vizuri zaidi iwapo kuna maji ya kutosha kwenye udongo. Mwagilia mara mbili au zaidi kwa wiki kutegemea hali ya hewa na aina ya udongo. Kabichi ambazo hazikupata maji ya kutosha huchelewa kufunga na huwa na vichwa vidogo. Zikikosa maji kwa muda mrefu na zikapata maji mengi ghafla, vichwa hupasuka. 

 MBOLEA
Mbolea ya kukuzia (S/A) huwekwa baada ya 4 – 6 baada ya kupandikiza miche na kabla ya vichwa havijaanza kufunga. Kiasi cha kilo 80 huhitajika kwa eka moja. - Kilo 40 ziwekwe baada ya wiki 4 – 6 na kilo 40 ziwekwe tena baada ya mwezi mmoja . Mche mmoja huhitaji kiasi cha kidogo cha gramu 5. Mbolea iwekwe kuzunguka shina umbali wa sentmita 10 – 15 kutoka kwenye shina. Muhimu: Epuka kuweka mbolea nyingi, kwani husababisha vichwa visifunge vizuri (kabichi zinakuwa nyepesi) 

 KUBADILISHA MAZAO
 Kabichi nizao linalotumia virutubisho vingi kulinganisha na mboga nyingine,hivyo kabla ya kuotesha kabichi panda mazao jamii ya mikunde ili kuongeza rutuba. Baada ya kuvuna kabichi otesha mazao yanayotumia chakula kidogo kama vile karoti, radishi au lettuce. Kubadilisha mazao pia hupunguza kuenea kwa wadudu waharibifu na magonjwa. 

KUVUNA
 



 Kabichi hukomaa katika siku 60 mpaka 210 tangu kupandikiza miche. Hata hivyo muda wa kukomaa hutegemea aina ya kabichi. Uvunaji hufanyika kwa kukata shina sentimita 2 – 3 kutoka kwenye kichwa kwa kutumia kisu. Ondoa majani ya nje na acha majani 2 au 3 ya kijani kwa ajili ya kuzuia kabichi zisikwaruzike na kuoza wakati wa kusafirisha. Punguza urefu wa majani ili kurahisisha ufungaji. Ni muhimu uvunaji ufanyike asubuhi au jioni. Ondoa kabichi zilizooza au kuharibika wakati wa kuvuna, kisha panga zilizobaki kufuata daraja kama vile ndogo, za kati na kubwa. Mavuno: Kiasi cha tani 40 au zaidi za kabichi hupatikana kwa hekta moja kama zao limetunzwa vizuri.

HIFADHI
Kabichi ni zao linaloharibika kwa haraka, hivyo halina budi kutumika mapema iwezekanavyo baada ya kuvuna. Kabichi kwa ajili ya kuuzwa zisafirishwe mara moja kwa walaji. Kama usafiri ni mgumu, zihifadhiwe kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha. Wakati wa kusafirisha, ziwekwe kwenye matenga au visanduku vya mbao vilivyo na matundu yanayoingiza hewa ya kutosha. leo tuishie hapa unaweza kuandika chochote au kutoa ushauri

No comments:

Post a Comment