Thursday, March 24, 2016

WADUDU WAHARIBIFU NA MAGONJWA MBALI MBALI KATIKA ZAO LA KABICHI


 







WADUDU WAHARIBIFU
 Viwavi wa kabichi: Hawa ni viwavi wenye rangi ya kijani na alama ya mstari wa kung’aa mgongoni. Nondo hutaga mayai chini ya jani na baada ya kuanguliwa viwavi hawa hula sehemu ya chini ya jani na kucha ngozi nyembamba mfano wa dirisha la kioo. Ni muhimu kuwadhibiti viwavi hawa kwa sababu ndio wanaoleta madhara makubwa. Viwavi wa kabichi huzuiwa kwa kunyunyizia moja ya dawa zifuatazo:- Nogos, Permethrin,Dimethoate, Sevin W.P. na Sumicidin.
 
Nzi wa Kabichi: Mashambulizi hufanywa na kiluwiluwi mwenye rangi ya kijani au bluu. Hula majani yote ya kabichi na kubakisha vena au vishipa vya majani. Inzi wa kabichi wanaweza kuzuiwa kwa kutumia dawa za Sevin, Dimethoate, Permethrin na Fenvalerate(sumicidin)

 Sota: Hawa ni funza wakubwa wenye rangi ya kijivu. Hupendelea kujichimbia katika udongo wakati wa mchana na kukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi wakati wa usiku. Zuia wadudu hawa kwa kutumia majivu au dawa kama vile Carbaryl, Fenvalerate au Decis mara baada ya kuotesha. Kama mche utakatwa, mtoe mdudu huyu kwa kumfukua na kumuua. Kisha pandikiza mche mwingine. 

Vidukari au wadudu mafuta:  Wadudu hawa ni wadogo sana wenye rangi ya kijani, nyeusi au khaki.  Baadhi yao wana mabawa na wengine hawana. - Hufyonza utomvu wa mimea na husababisha majani kubadilika rangi na kuwa meupe au njano iliyopauka.  Mmea hudumaa na hatimaye hukauka. Zuia kwa kunyunyiza mojawapo ya dawa hizi Fenvalerate, Dimethoate, Karate, Nogos

Minyoo Fundo: Ni minyoo wadogo wanaoishi ardhini na ambao hawaonekani kirahisi kwa macho. Hushambulia mizizi na kusababisha kabichi kudhoofu na kushindwa kufunga vizuri. Mimea iliyoshambuliwa, mizizi yake huwa na nundunundu. Kuzuia: Matumizi ya mbolea za asili kila msimu husaidia kupunguza kuzaliana kwa wadudu hao. - Tumia mzunguko wa mazao, usiotesha zao la jamii ya kabichi baada ya kuvuna kama vile kabichi ya kichina, koliflawa,n.k Otesha mboga kama vile karoti, radishi, vitunguu au mahindi. - Ondoa masalia yote shambani ambayo yanaweza kueneza wadudu hawa na yachome moto.

 MAGONJWA

 Kuoza shingo; Husababishwa na vidudu vya bacteria ambavyo viko kwenye udongo. Hushambulia kabichi na kuzifanya zibadilike rangi.  Kuoza na kutoa harufu mbaya. Vidudu vidovidogo huonekana pia kwenye sehemu iliyooza. Kuzuia:
·        Epuka kujeruhi kabichi wakati wa kuvuna.
·        Vuna kabichi wakati hakuna mvua - Usilundike kwa wingi na kwa muda mrefu.
·         Hifadhi kwenye sehemu yenye ubaridi na hewa ya kutosha.
·        Ng’oa masalia, choma moto na lima shamba mara moja baada ya kuvuna - Tumia mzunguko wa mazao. 

 Uozo Mweusi;  husababishwa na Bakteria . Majani hugeuka kuwa njano na baadaye kuwa kahawia . Majani huanza kunyauka kutoka kwenye kingo zake na kuacha alama ya “V” yenye rangi nyeusi isiyokolea.  Baadaye majani hunyauka na kupukutika. Kama ukikata jani au shina, mviringo mweusi huonekana kwenye vena.
Kuzuia:
·        Badilisha mazao.
·        Usipande kabichi au jamii yake kwa muda wa miaka 2 kwenye eneo lililoadhirika.
·        Otesha kabichi kwenye sehemu ambayo haituamishi maji.
·         Kitalu na mazingira yake viwe safi daima.
·        Punguza miche ili kupunguza msongamano.
·         Ondoa masalia yote baada ya kuvuna ya yachomwe moto.
·        Otesha mbegu zilizodhibitishwa na wataalam.

 Kuoza shina; Ni ugonjwa waukungu, Madoadoa yaliyodidimia yenye rangi ya kahawia huonekana kwenye shina karibu na usawa wa ardhi, ikifuatiwa na kuvimba kwa shina.  Baadaye uyoga mweusi huonekana kwenye uvimbe huo. Uozo wa rangi ya kahawia huonekana ndani ya shina.  Majani huwa na madoa meusi ya mviringo yaliyozungukwa na uyoga mweusi.
 Kuzuia:
·        Otesha kabichi sehemu ambayo haituamishi maji.
·         Badilisha mazao, usioteshe kabichi kwenye eneo lililoathirika kwa muda wa miaka 3.
·         Lima shamba mara baada ya kuvuna ili kuwezesha masalia kuoza haraka kabla ya kuotesha tena.
·         Ondoa kabichi zote zilizoshambuliwa shambani.
·        Tumia dawa ya kuzuia ukungu kama vile Ridomil. 

 Uvimbe wa mizizi; Husababishwa na ukungu. Hushambulia mizizi na dalili zake ni kudumaa kwa mmea na majani kukunjamana . Baadae mmea huoza
Kuzuia: Badilisha mazao shambani.

Madoa Meusi:  Chanzo ni ukungu. Majani huwa na madoa madogo madogo ya mviringo yenye rangi ya njano .  Baadae madoa huwa makubwa na hugeuka kuwa meusi.
Kuzuia:
·        Badilisha mazao
·         Hakikisha shamba ni safi wakati wote
·         Ikibidi tumia dawa za ukungu kama vile Kocide,Cupro, n.k. ·
·        Ubwiri

 Vinyoya:  Ni ugonjwa wa ukungu. Hupendelea hali ya unyevunyevu na baridi kali. Huanzia kwenye kitalu . Mabaka ya mviringo yenye rangi ya njano huonekana upande wa juu wa jani. Baadae hubadilika na kuwa rangi ya zambarau iliyochanganyika na nyeupe upande wa chini wa majani.
Kuzuia:
·        Tumia mzunguko wa mazao.
·        Hakikisha udongo hautuamishi maji na kitalu ni kisafi wakati wote.
·         Tumia za ukungu kama Zineb, Didhane, M45, Kocide, Topsin-M na Ridomil.

Kuoza shina au Kinyaushi: Husababishwa na ukungu. Hushambulia miche michanga. Miche iliyoshambuliwa huonyesha dalili za kukauka. Miche mikubwa huonyesha dalili za kudumaa. Sehemu ya shina iliyo karibu na ardhi hulainika na kuwa rangi ya kahawia.
Kuzuia:
Punguza miche kama imesongamana. Nyunyiza dawa ya ukungu Kama Didhane M-45, Ridomil, Topsin-M.

No comments:

Post a Comment