WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali aende
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ili akague taarifa za mapato ambazo zilikuwa
zikilipwa na mawakala wa forodha na bandari kupitia benki ya CRDB lakini hazionekani
kwenye mifumo ya benki.
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Jumatatu, Machi 17, 2016) wakati akizungumza na mamia ya mawakala
wa forodha na bandari waliohudhuria mkutano aliouitisha ili kusikiliza kero
zinazowapata katika utendaji kazi wao.
Akizungumza
na mawakala hao kwenye ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu
alisema kuna dalili za kutupiana lawama baina TPA na CRDB kuhusu malipo
yaliyikuwa yakifanyika benki halafu fedha hazionekana na wakala anaidaiwa kuwa
hajalipia mzigo wakati alishaulipia.
“Kimsingi
bado liko tatizo baina ya Mamlaka ya Bandari pamoja na Benki ya CRDB. Naona
kila mmoja hapa anamkana mwenzake. Nitamtuma CAG ili akafanye ukaguzi wa kina
ili tujue ni nani kati yao amehusika na upotevu wa fedha,” alisema huku
akishangiliwa na mawakala hao.
Alimwagiza pia
Kaimu
Mkurugenzi wa Bandari, Eng. Aloyce Matei aandae dispatch zote walizotumia kupokelea malipo za kuanzia mwaka 2015 na
ikibidi aandae za kuanzia mwaka 2014 ili CAG anapozopitia aweze kupata picha
halisi.
Vilevile, Waziri Mkuu alimwagiza Eng.
Matei kuhakikisha wananunua mashine ya photocopy ili iwekwe kwenye chumba cha kupokelea
stakabadhi za malipo ya benki (bank pay in slip) ili mteja anapoleta nakala ya
benki aweze kutolewa photocopy na kubakia na nakala ya malipo aliyofanya,
Waziri Mkuu alisema Serikali
inatambua bandari ni eneo nyeti katika kuinua uchumi na mapato ya nchi lakini
pia ni eneo muhimu katika kutengeneza ajira. “Ninapenda niwahakikishie kuwa bado
tutaendelea kukagua bandari hadi pawe safi. Hii bandari ni yenu na mtafanya
kazi kama kawaida,” alisema.
Mapema, akizumgumza kwa niaba ya
mawakala hao, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha nchini (TAFFA), Bw. Stephen
Ngatunga alieleza matatizo mbalimbali ambayo wao kama mawakala wa forodha
wamekuwa wakikumbana nayo kuanzia ulipaji, utoaji wa mizigo na kuitaka Serikali
iongeze nguvu katika kuikabilia sekta hiyo.
Alizikosoa baadhi ya sheria ambazo zinaruhusu
wamiliki wa bandari kavu kumiliki pia makampuni ya uwakala wa forodha, sheria kadhaa
zinazochangia kukwamisha utoaji wa mizigo bandarini, ukaguzi hafifu wa kwenye scanner
na uwepo wa vituo vinane vya mizani kuanzia Dar es Salaam hadi Tunduma ambavyo
vimegeuka kuwa kero kwa wasafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Wakati
huohuo, Naibu
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani amesema Serikali
imeamua kuyafungulia makampuni zaidi ya 150 ambayo yalikuwa yamefungiwa kufanya
kazi za uwakala wa forodha kutokana na madai ya kuhusishwa na ukwepaji wa kodi.
“Hapa tumegundua kuwa wote siyo
wasafi iwe ni mawakala, benki ama bandari. Mkurugenzi wa Bandari, kuanzia leo
watu hawa waruhusiwe waanze kufanya biashara lakini nyaraka za nyuma zisiguswe
hadi CAG atakapokamilisha uchunguzi wake,” alisema kuibua kelele za shangwe
kwenye ukumbi huo.
No comments:
Post a Comment