Thursday, March 24, 2016

MADHARA YA KUTUMIA KEMIKALI NYINGI SHAMBANI KWAKO







Wakulima wamekuwa wakitumia kemikali kiasi cha kutisha kwenye mazao kwa ajili ya kudhibiti wadudu.
Kwa mfano uzalishaji wa nyanya unaweza kuwa na faida kwa mkulima. Msimu ambao nyanya zinakuwa chache bei hupanda mkulima anapata faida zaidi. Kwa upande mwingine zao la nyanya ni rahisi sana kushambuliwa na wadudu na magonjwa.
Tatizo moja kubwa la kutumia dawa za kudhibiti wadudu na magonjwa  kwa kiasi kikubwa ni kuwa wadudu hao huwa sugu baada ya muda mfupi. Wakulima kwa uoga wamebuni njia yao wenyewe ya kudhibiti wadudu na magonjwa. Imetushangaza na kutushtua kugundua kuwa baadhi ya wakulima hapa nchini wanatumia dawa ya kuulia kupe kwa ajili ya kuua wadudu wa nyanya kama vile inzi weupe, vithiripi, utitiri na buibui.
Dawa hii inaruhusiwa kutumika kwa ajili ya kuogeshea wanyama tu lakini si kwenye mboga ambazo zinauzwa kwa walaji.
Sokoni kuna aina nyingine za dawa ambazo ni hatari na zilishapigwa marufuku na serikali, lakini cha kushangaza baadhi ya maduka ya pembejeo bado yanaziuza na wakulima wanatumia.
Aina hizi za kemikali ni hatari sana kwa afya ya binadamu hasa zinapojikusanya kwa kiasi kikubwa mwilini. Baada ya muda mrefu inaweza kuwa sugu na kusababisha magonjwa ambayo pia ni sugu ambayo hata sasa yamekuwa tatizo kubwa katika baadhi ya maeneo hapa nchini, kwa mfano saratani, ukuaji usiokuwa wa kawaida kisukari na magonjwa ya mzio.

Mbali na madhara kwa afya ya binadamu, pia sumu hizo hupenya na kwenda kwenye maji yaliyomo ardhini na kuyachafua. Sumu hizo huathiri na kuuwa wadudu muhimu waliomo ardhini ambao huboresha udongo, kuuwa wadudu muhimu ambao hufanya ushavushaji kwenye mazao, na wadudu wengineo ambao hudhibiti wadudu waharibifu kwenye mazao na mazingira yetu.

Njia endelevu za kudhibiti wadudu
Kuna mbinu za kudhibiti wadudu ambazo ni salama kwa mazingira yetu. Njia hizo zinajumuisha matumizi ya wadudu rafiki kama vile nyigu, bungo na wengineo kwa ajili ya kudhibiti wadudu hawa.
Endapo wakulima wataacha kutumia kemikali hizi, wadudu hawa wataweza kudhibiti wadudu hao waharibifu kwa asili. Endapo madhara makubwa mkulima anaweza kutumia dawa za asili katika kudhibiti wadudu hawa, dawa ambazo hazina madhara yoyote.

Tumia dawa za asili
Mojawapo ya wadudu ambao huwa wakulima hupata shida kuwadhibiti, ni inzi weupe, vithiripi, buibui wekundu, na vidukari. Wadudu hawa huharibu kati ya asilimia 20-30 ya mazao na kuendelea. Wadudu kama vithiripi na inzi weupe ni vigumu sana kuwadhibiti kwa kuwa huzaliana kwenye mazao yanayokua. Hivyo tumia njia ya  kujihami kabla.
Badala ya wakulima   kutumia kemikali, wanaweza kutumia dawa za asili ambazo haziui wadudu rafiki na ambazo pia husaidia mimea kujijengea kinga dhidi ya magonjwa.

Kuandaa dawa za asili:
Mkulima  anaweza kutumia aina nyingi za  mimea katika kutayarisha dawa za asili.  Mfano wa mimea hiyo ni pamoja na bangi mwitu, tangawizi, mlonge, Mwarobaini na pareto. Katakata mimea  yote hiyo kwenye debe na uloweke kwenye pipa lenye ujazo wa lita 200.
Jaza maji kwenye pipa hilo na uchanganye kwa nguvu sana. Funika pipa hilo vizuri uhakikishe hakuna hewa inayopita. Ongeza lita moja ya EM na lita 4 za molasesi. Vundika kwa muda wa siku 7-10. Weka mchanganyiko wa mimea ya dawa kwenye bomba la lita 20 lililojazwa maji. Nyunyiza kwenye mazao yako angalau mara tatu kwa wiki. Dawa za asili zinaweza kukinga mazao yako dhidi ya wadudu wote na hata magonjwa, pamoja na kupata mazao ambayo ni salama kwa afya.

No comments:

Post a Comment